Serikali
imepiga marufuku matumizi ya Barua pepe za kawaida kwa watumishi wa
umma wanaotuma au kupokea taarifa za Serikali na kuwataka watumishi hao
kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo rasmi wa Mawasiliano ya Barua Pepe
Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha
mawasiliano kwa njia ya Mtandao.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angella Kairuki alipokuwa
akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao ( e
Government Agency) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji na ufanisi
wa matumizi ya TEHAMA Serikalini.
“Sasa
kuna watumishi 7000 wanaotumia anwani za Barua pepe za Serikali ,idadi
hii ni ndogo lazima iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa
taarifa za Serikali kwa kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huu” Amesisitiza na kuongeza kuwa Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye mawasiliano binafsi.
Amesema
kwa kutambua umuhimu wa uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA Serikalini
na kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia
mitandao mbalimbali ipo haja ya kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma
kutumia Barua Pepe za Serikali.
Mhe.
Kairuki amewataka watendaji wa Wakala hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia
uratibu wa zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa Wizara, Idara na Taasisi
zote za umma zinaunganishwa na mfumo rasmi wa Serikali ili kuwa na
mfumo mmoja wa Mawasiliano.
“Katika
hili ninatoa siku 60 muhakikishe kuwa mnakamilisha kwa Taasisi
zilizobaki ili kwa wale watakaopuuzia hatua zianze kuchukuliwa” Ameeleza Mhe. Angella.
Aidha,
ametoa wito kwa watendaji wa Wakala hiyo kuweka mpango wa kuwawezesha
na kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi waliopo kazini kwa kujenga
utaratibu wa kuwarithisha uzoefu watumishi ili kuendelea kuimarisha
ufanisi na utendaji wa Wakala hiyo.
Mhe.
Kairuki amewataka kuwa wabunifu katika kuanzisha mifumo mipya ya
TEHAMA ili kuimarisha dhana ya Serikali mtandao ili kupunguza gharama
hadi kufikia asilimia 5 ya fedha zinazotumika kuendeshea masuala
mbalimbali ambayo yangefanywa kupitia matumizi ya TEHAMA.
Akizungumzia
kuhusu ununuzi wa vifaa vya TEHAMA serikalini ameitaka Wakala hiyo
kutoa ushauri ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya
fedha katika kununulia vifaa hivyo kwa gharama kubwa wakati vinaweza
kupatikana kwa bei ya kawaida.
“katika
hili Serikali itachukua hatua kwa yeote atakayebainika katika upotevu
wa mapato muhakikise mnazisaidia Wizara na Taasisi mbalimbali za
Serikali katika masuala ya ununuzi wa mifumo na vifaa vya TEHAMA ili
mifumo inayonunuliwa iwe na manufaa kwa wananchi na thamani halisi ya
fedha”
Amesema
Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa huduma kupitia mtandao ili
wananchi waweze kupata huduma hizo mahali walipo kwa gharama nafuu na
kutoa wito kwa watumishi wa Wakala ya Serikali mtandao (e-Gov) kuwa
wabunifu katika kutengeneza programu mbalimbali na mifumo salama
itakayowasaidia wananchi kupata huduma.
Aidha,
katika hatua nyingine ameitaka e-Gov kuendelelea kujenga uwezo katika
kudhibiti dharura na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza katika
matumizi ya TEHAMA na kuitaka Wakala hiyo iendelee kulifanyia kazi suala
la kuwezesha mifumo ya Serikali kuzungumza kati ya taasisi moja hadi
nyingine ili huduma zote ziweze kupatikana katika eneo moja na kuondoa
urudufu wa mifumo iliyopo.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (e-Gov) Dkt.
Jabiri Bakari akitoa taarifa ya utendaji wa Wakala hiyo amesema kuwa
licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali toka kuanzishwa kwake Julai
11, 2012 imeendelea kupata ufanisi katika uimarishaji wa Serikali
Mtandao.
Amesema
kuwa Wakala hiyo inaendelea kuhakikisha kuwa huduma za Serikali
zinawafikia wananchi kupitia mtandao mahali walipo na kuhakikisha kuwa
inafanikisha lengo la huduma zote za Serikali kupatikana chini ya
dirisha moja.
Aidha
amesema kuwa Wakala ya Serikali Mtandao itaendelea kuhakikisha kuwa
usimamizi wa viwango vya matumizi ya TEHAMA katika Idara na Taasisi
mbalimbali za Serikali unazingatiwa.